Jeshi la polisi mkoani Tabora lalamikiwa kuwapendelea wachina
Written By Voice of Tabora Radio on Monday, May 20, 2013 | 9:55 PM
Mkuu wa wilaya ya Uyui bi. Lucy Mayenga ametembelea wodi namba moja ya hospitali ya mkoa wa Tabora Kitete kumjulia hali mfanyakazi wa kampuni ya ujenzi wa barabara ya Tabora - Nyahuwa CEFTEC bwana Alex Semindu ambaye amelazwa kufuatia kupigwa na kujeruhiwa na walinzi wa kampuni hiyo.
Baada ya kumuona mfanyakazi huyo mkuu wa wilaya alielekea kambi ya Inala inayomilikiwa na kampuni hiyo ambapo alipata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi wazalendo.
Wafanyakazi hao wamezitaja kero zao kuwa ni pamoja na jeshi la polisi mkoani hapa kuwakamata na kuwaachia watuhumiwa walioshiriki kumpiga na kumjeruhi bwana Semindu wakati akiwa bado amelazwa hospitalini.
Kero nyingine iliyotajwa ni pamoja na jeshi hilo la polisi kuwapendelea wachina wanapofika kituoni na kuwapuuza wafanyakazi wa kitanzania jambo ambalo linawanyima haki wazawa.
Wafanyakazi hao wasema kampuni ya CEFTEC haitoi mikataba ya ajira kwa wafanyakazi na wamekuwa wakikatwa malipo ya mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF kwa zaidi ya miezi mitano pasipo kusajiliwa na mfuko huo na wanapohoji wanaambiwa waache kazi.
Aidha wafanyakazi hao wamemwambia mkuu huyo wa wilaya ya Uyui kuwa kero nyingine waliyonayo ni wafanyakazi hao kukatwa kiasi cha shilingi elfu 40 kila mmoja kama gharama za vifaa vya kutendea kazi jambo ambalo ni wajibu wa kampuni hiyo.
Hata hivyo bi Lucy Mayenga amewaambia wafanyakazi hao kuwa na subira wakati serikali inazitafutia ufumbuzi kero zao.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !